AFRIKA ZAMANI |
Hapo zamani za kale, zamani sana kitambo nizaliwe mimi... labda hukuwepo pia wewe,
Mababu zetu waliishi vyema, wakishauriana kuhusu kila jambo ambalo wangetekeleza kama jamii. Nafurahia kwa namna ambayo majukumu yalitekelezwa kwa umoja na ushirikiano mkubwa wa kijamii.
Nilipokuwa nikivisoma vitabu vya hadithi za kale, kuna baadhi ya mambo ambayo yalijitokeza wazi kila niliposoma vitabu vilivyotungwa na waandishi kuhusu matukio na jamii ya mwanzoni mwa Afrika, niliweza kufahamu kuwa UPENDO NA USHIRIKIANO WA KIJAMII ndio uliokuwa haswa kioo cha jamii.
Tunzo za kale zilishamiri mafunzo kwa msomaji kiasi cha kwamba ungeweza kufaidika kama msomaji kunukuu baadhi ya maneno aliyotumia mwandishi ukayatumia kujijenga binafsi. Aidha, msomaji angewza kujifunza kuhusu maudhui yaliyolengwa vyema na mtunzi wa makala, kwa mfano Mwandishi angelenga kuandika kuhusu nidhamu, tamaduni, bidii, ukulima n.k, Maudhui haya yangejitokeza vyema katika fasihi ili kumnufaisha msomaji.
Mbali na kupitia mbinu ya FASIHI ANDISHI, mbinu nyingine ambayo ilitumika vyema sana nyakati za utoto wetu ni mbinu ya FASIHI SIMULIZI. Mbinu hii haswa iliwafaidi watoto ambao kwa kiwango fulani hawangeweza/hawakuwa na ule uwezo wa kutumia fasihi andishi,
Katika fasihi hii, wazee katika familia wakiwemo mababu pamoja na Mabibi(Nyanya) waliwakusanya vizazi vyao wakawahadithia hadithi za kale.
Watoto Wakihadithiwa hadithi za kale-Afrika |
Hadithi ambazo mababu zetu walihadithiwa na watangulizi wao, nao wakazipitisha hadi kwa wanao na hatimaye kwa vizazi vingine vichanga. Katika hadithi hizi, mawaidha yalipeanwa kuhusu jinsi mwana anastahili kujiheshimu na kutekeleza majukumu ya jamii.
Kwa mfano, mtoto wa kike angefunzwa majukumu ya kike, kila siku jioni wakati wa maandalizi ya chakula cha jioni kule jikoni, Mama/Nyanya/Shangazi angewakusanya watoto wasichana akaketi nao jikoni na kuwafunza baadhi ya mambo ya kike wanapoandaa chakula kwa jamii. Mfumo huu uliwafaa sana kwa kuwa ulikuwa mtindo wa kuwalea watoto na kuwapa maandalizi ya siku za usoni.
Kwa upande mwingine, Babu/Baba/Mjomba angewakusanya watoto wa jinsia ya kiume, wakaketi nje, chini ya mti, wakawasha mtoto na kuketi kandokando wakahadithiwa hadithi za kale. Mara nyingi hadithi hizi zilikuwa za kishujaa na kuonyesha jinsi mtoto wa kiume alivyokuwa ngome katika kuilinda jamii wakati wa vamizi..
Uvamizi wakati ule haukuwa wa Bunduki wala mabomu, watu walijifunza kujikinga na kuikinga familia kutokana na uvamizi wa Majitu na wanyama wa mwituni kama vile Fisi ambao walivamia na kuwala mifugo wa jamii.
FISI-Wanyama waliowavamia na kuwala mifugo katika jamii |
Mtoto wa kike alifunzwa mambo mengi yaliyohusu kuilinda jamii mbali na kuwa mwazo wa kuendeleza uzao wa familia.
Mafunzo haya yaliwafaa wanajamii kwa kiasi kikubwa kwamba jamii ilikuwa na watu ambao walikuwa watiifu wakazingatia itikadi za jamii na kufuata mila za jamii.
Natamani kuwa na Afrika ya zamani, Afrika ambayo tuliishi kwa undugu, hatukujua kabila wala dini
Natamani...
Na William Khaemba
Mwanahabari-Mbunifu
Barua pepe : khaemba80@gmail.com
Facebook : William Khaemba
Google : +William Khaemba
Twitter : @Khaemba_KE
Mobile : +2547-17-213-561